LYRICS

Dizasta Vina – Hatia IV Lyrics

Dizasta Vina – Hatia IV Lyrics
Dizasta Vina – Hatia IV Lyrics

“JASIRI JOHN….. ALIYAANGALIA MAISHA YAKE
HAKUONA JINSI ANGEWEZA KUISHI BILA JANE
MSICHANA ANAYEMPENDA
LICHA YA KUZONGWA NA UMASIKINI
ALIJITAHIDI KUMPA JANE MAHITAJI MADOGOMADOGO KADRI ALIVYOWEZA

LAKINI ALIFAHAMU SHUBIRI YA KUSUBIRI KUPENDWA HUKU ANAFAHAMU KUSUBIRI KUPENDWA NI MATUMAINI YANAYOUMIZA. KAMA WANAVYOSEMA, MTAFUTAJI HACHOKI AKICHOKA KASHAPATA….ALIENDELEA KUNGOJA”

Ah! Sikuwa na zali sikuziamini ndumba
Sikuwa na mali za kufuja
Nilijitahidi kuuza mitumba kufuga mipunga
Ili siku nimpe gari nimpe nyumba. Nilishindwa…
Niliishia kumpa chai, ‘chipsi’ mayai na ‘vocha’
Nywele za kimasai na mkoba
Pesa za magauni, majuba na viatu vya kuzuga
Nilimpa muda ila bado haikutosha, kwani…

Nilipomwambia nampenda hakujibu
Akaweka moyo wangu maumivu
Na mtima wangu akauweka ‘solemba’
Nikaapia kuwa sitakuja kupenda ‘forever’

Ah! Nilimpa upendo nilimpa sifa
Niliweka mitego ya faida, haikuwa shwari
Nikabadili mwenendo wa maisha
Niliweka malengo sikutimiza, hakunikubali

Alikuwa na ndoto kubwa kushinda mimi
Alikuwa na misimamo kuipita dini
Aliniambia ameomba nije kuokota utajiri
Amengoja sana na sasa amechoka kusubiri

“JOHN ALIFAHAMU HALI YA JANE, KUWA JANE ALIZALIWA KWENYE
FAMILIA MASIKINI, NA ALIUCHUKIA MNO UMASIKINI. ALIFAHAMU UMASIKINI ULIVYOCHUKUA UHAI WA MAMA YAKE KIPENZI, ALIYEFARIKI KWA KUKOSA MATIBABU. ALIIFAHAMAU NADHIRI ALIYOIWEKA JANE YA KWAMBA HATOKUBALI TENA KUISHI KWENYE MAISHA YA KIMASIKINI, NADHIRI ILIYO MWEKA JOHN NJIAPANDA”

Ah! Sikuwa na hali ya kuikosha roho yake
Nilimwacha aende aufate moyo wake
Alipata bwana wa kizungu magharibi
Alimwahidi kuishi maisha ya ndoto zake

Nilipata uchungu niliishia kuhamaki nilitaka nijiue
Nilitaka nimzuie abaki nikakumbuka
Ukipenda ua haulikati unaliacha likue

Duka langu nilifunga biashara niliacha zote
Uchumi uliyumba kwa maana nilianza pombe
Niliumwa bado kidogo moyo uzime
Nilimfanya ndoto kumbe naye ana ndoto nyingine

Alisema anakwenda jiji la Miami
Hakuna alichowaza zaidi ya kuishi kifahari
Kamtumia picha na ‘mchizi’ kazikubali
Na yupo tayari kumlipia gharama za safari

Aliondoka na kipande kimoja cha mwili
Nilikonda nilipata ugonjwa wa akili
Haikuwahi kupita hata sekunde nisilie
Nilitamani mpaka ardhi ipasuke niingie

“JANE ALIPOONDOKA ALIMWACHIA JOHN KIDONDA KILICHOCHELEWA SANA KUPONA
NA YEYE AKAWEKA NADHIRI YA KUTOJIHUSISHA NA MAPENZI TENA MAISHANI MWAKE. ALIKAA KWA MUDA MREFU BILA MAHUSIANO. LAKINI…
HAKUNA DAKTARI MZURI KAMA MUDA, JOHN ALIPONA MAUMIVU NA ALIIRUDIA HALI YAKE YA KAWAIDA”

Ah! Muda ukaenda nitapata ‘Mwanamwali’
Nikamwomba awe mwenza wa maisha akakubali
Nikamvisha pete nikalipia mahari
Sikumpenda lakini nilijifunza kumjali
Aliuliza kama nampenda, nilimjibu
Sikutaka kuweka moyo wake maumivu
Sikutaka kuuweka Mtima wake solemba
Kiasi aseme hatakuja kupenda ‘‘forever’’

Ah alinikumbatia nikamfunga kwa ishara
Akanikabidhi tunda nikala
Akaniamini tukajuana nikapanga kumwoa
Akaidhisha na tukaanza na mipango ya ndoa

“WAKATI KARNE YA 21 INAINGIA, JOHN ALIKUWA NI MIONGONI MWA
VIJANA WALIOKUWA ‘FASCINATED’ NA UKUAJI WA TEKNOLOJIA YA MITANDAO YA KIJAMII. ALIJIUNGA NA DUNIA HII MPYA, MARA KADHAA ALIKAA KWENYE UBARAZA, AKIANGAZA SIMU YAKE. AKIPAPASA KILA KITUFE, NDIPO SIKU MOJA AKAPATA UJUMBE KUTOKA KWA JANE”

“Habari naamini u bukheri wa afya
Unaendeleaje maisha na huyo mpenzi wa sasa
.nashukuru nahema ughaibuni si kwema
Nakiona cha mtema mpaka naona ni heri nikafa…

Ah! Maisha niliyowaza yote ni uongo
Nauzishwa madawa nalazimishwa ngono
Nafungiwa ndani kama mtumwa ufungwani
Roho yangu rehani kiasi sasa naitamani Bongo

Ukubwa umekuja kunisafisha jicho
Ndoto imeisha na taswira imenionyesha sivyo, ah
Naomba unifate uniondoshe kwenye hichi kifo
Na hii namba ya msamaria atakueleza nilipo”

Sherehe ilikuwa na mipango madhubuti
Kabla mimi kuichukua michango ya Harusi
Nikatoroka ughaibuni kufuata hisia zangu
Kwenda kumfata njiwa wangu mahususi

Nilivuka majangwa na majabali
Sehemu ya safari anga sehemu nyingine bahari
Niliacha kila kitu nyuma upendo na huruma vilinijaa
Penzi likanipeleka mbali

“JOHN ALIFIKA UGHAIBUNI, AKAMTAFUTA MSAMARIA ALIYETAMBULISHWA NA UJUMBE, MSAMARIA AKAMWELEKEZA NJIWA WAKE ALIPO, NA NIKWELI… HAPAKUWA PEMA”

Nikakutana na bopa la kizungu
Lenye sura ya kuichachisha mboga kwenye chungu
Kiko kwenye mdomo,Tatuu kila kona na wapambe
Pamoja na vishoka wenye mtutu

Sio siri alizungukwa na wasichana wengi
Sikujua umri walikuwa wadogo ka’ “madent”
Baadhi walikuwa uchi wanahesabia “chenchi”
Wengine masaji huku wengine wanamchezea nyeti

“MASIKINI JOHN, ALIDANGANYA KWA KUJITAMBULISHA KAMA KAKA KWA JANE, AKIMSIHI YULE MAFIA AMRUHUSU AONDOKE NA JANE WAKAANZE MAISHA MAPYA, LAKINI… PALIPOSHINDWA SHOKA WEMBE HAUWEZI TAMBA. KWA KUZIDIWA NA UOGA WA KUUAWA…JANE ALIMKANA JOHN KWA KUSEMA HAMJUI…”

Hata nilipomuuliza kama ananipenda hakujibu
Akaweka moyo wangu maumivu
Nilijua hawezi kufa kwa sababu hakunipenda
Na ni rasmi nikapoteza shilingi kwenye msitu

Nilikiambia kifo kama unakuja njoo
Maana sikuwa mtu ilishakufa roho
Sikuumia kama alivyoniumiza yeye
Kwahiyo sikujali jinsi nilivyoteswa na wale mbwa no

Aliambiwa ambusu bosi hakubisha
Alipewa bunduki hakusita
Aliishika risasi akaiingiza
Akaambiwa anipige kwenye kichwa

JOHN ALIKUWA NI JINA JIPYA LA WAHANGA WA UPENDO WA DHATI, VIPOFU WA MAPENZI, WAJINGA WA MAHABA…

JOHN ALIKUWA ROMEO KWENYE ROMEO AND JULIETH, ALIKUWA SAMSON KWA DELILAH KWENYE WAHUKUMU WA AGANO LA KALE, ALIKUWA JACK KWENYE TITANIC, FRED WEASLEY KWENYE HARRY POTTER..

JOHN ALITUKUMBUSHA KUWA UPENDO NI SADAKA, SADAKA YA MUDA NA PESA, ALITUKUMBUSHA UPENDO NI SADAKA YA DAMU

JOHN, ALIPOTEZA UHAI AKIWA KWENYE SAFARI YA KUTAFUTA UPENDO WA MTU ALIYEMHUSUDU NA
JANE ALIPOTEZA AMANI NA THAMANI YAKE KAMA MTU AKIWA KWENYE SAFARI YA KUTAFUTA UTAJIRI ALIOUHUSUDU

Hatia iko wapi?

Leave a Comment