ENTERTAINMENT

Kwa Heshima ya Eng. Hersi, Nibaki Yanga – Aziz Ki

Kwa Heshima ya Eng. Hersi, Nibaki Yanga - Aziz Ki

Kiungo wa Yanga, Stephanie Aziz Ki, ameibuka kinara wa mabao Ligi Kuu ya NBC baada ya kufunga mabao 21, akimfunika kiungo wa Azam FC, Feisal Salum, mwenye mabao 19. Huku ndoto za Simba kushika nafasi ya pili katika ligi hiyo zikiota mbawa, Aziz Ki ameweka wazi msimamo wake wa kubaki Yanga.

RELATED: Wafungaji Bora Ligi Kuu | Top Scores NBC Premier League 2024

Kumekuwa na tetesi kuwa Aziz Ki amegoma kusaini mkataba mpya na Yanga kutokana na ofa kutoka timu kubwa barani Afrika zinazotaka saini yake. Hata hivyo, mwamba huyo kutoka Burkina Faso amevunja ukimya akisema hana mpango wa kuondoka Yanga msimu huu licha ya Eng. Hersi Said, Rais wa Yanga, kumtaka aondoke baada ya miaka miwili ya mkataba wake kufika mwisho.

“Siwezi kumpa zawadi yoyote Eng. Hersi kwa sababu amenipa vitu vingi sana tangu alipokuja kunichukua miaka miwili iliyopita. Alipokuja alinionesha ‘Aziz nina project hii, ninakuomba uje ufanye jambo kwenye timu yangu’. Niliheshimu project ya Rais na nikaja hapa kwa mkataba wa miaka miwili, ninaweza kuona project sasa inakoelekea na nina furaha sana,” alisema Aziz Ki.

Aziz Ki aliongeza kuwa aliahidiwa na Eng. Hersi kuwa baada ya miaka miwili atatafutiwa timu nyingine, lakini kutokana na furaha na mafanikio aliyoona ndani ya Yanga, ameona ni vyema kubaki kwa heshima ya rais wake. “Najua aliniambia baada ya miaka miwili niondoke, lakini sitaondoka nitaendelea kubaki kwa ajili ya heshima yake,” alisisitiza.

Kwa kumalizia, Aziz Ki alitoa shukrani zake kwa Eng. Hersi kwa nafasi aliyopewa na msaada aliompatia kuwa bora zaidi. “Asante sana kwa hii nafasi na asante kwa kila kitu kwa sababu umenisaidia sana kuwa bora na hii ni zawadi yangu kwako,” alisema Aziz Ki, huku akimkabidhi Eng. Hersi mpira aliozawadiwa baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Tanzania Prisons. Hata hivyo, Eng. Hersi alimwambia autunze mpira huo kwa ajili yake.

Kwa maneno haya, Aziz Ki amethibitisha tena kujitoa kwake kwa Yanga na kumuenzi Eng. Hersi kwa uaminifu na heshima kubwa.

Leave a Comment